1 Chronicles 12:23-40

Wengine Waungana Na Daudi Huko Hebroni

23 aHawa ndio watu waliojiandaa kwa ajili ya vita waliokuja kwa Daudi huko Hebroni ili kumtwalia ufalme kutoka kwa Sauli, kama Bwana alivyokuwa amesema:

24watu wa Yuda, wanaochukua ngao na mikuki walikuwa 6,800 wote wakiwa tayari kwa vita.
25Watu wa Simeoni, mashujaa waliokuwa tayari kwa vita walikuwa 7,100.
26Watu wa Lawi walikuwa 4,600, 27pamoja na Yehoyada, kiongozi wa jamaa ya Aroni, aliyekuwa pamoja na watu 3,700, 28 bna Sadoki, kijana shujaa na hodari, aliyekuwa pamoja na maafisa ishirini na wawili kutoka jamaa yake.
29 cWatu wa Benyamini, ndugu zake Sauli, walikuwa 3,000; wengi wao walikuwa wameendelea kuwa waaminifu kwa Sauli mpaka wakati huo.
30Watu wa Efraimu, mashujaa hodari 20,800, watu waliokuwa maarufu katika koo zao.
31Watu wa nusu ya kabila la Manase, waliotajwa kwa majina ili waje kumweka Daudi kuwa mfalme, watu 18,000.
32 dWatu wa Isakari, waliofahamu majira na kujua kile ambacho Israeli inapasa kufanya, walikuwa viongozi 200, pamoja na jamaa zao wote chini ya uongozi wao.
33Watu wa Zabuloni, askari wenye uzoefu mkubwa walioandaliwa tayari kwa vita wakiwa na silaha za kila aina, ili kumsaidia Daudi kwa uaminifu thabiti, walikuwa 50,000.
34Watu wa Naftali, maafisa 1,000, pamoja na watu 37,000 waliochukua ngao na mikuki.
35Watu wa Dani 28,600 waliokuwa tayari kwa vita.
36Watu wa Asheri, askari 40,000 wenye uzoefu mkubwa waliondaliwa kwa ajili ya vita.
37Na pia watu kutoka mashariki ya Yordani, watu wa Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase, wakiwa na kila aina ya silaha, watu 120,000.
38 eWote hawa walikuwa watu wapiganaji waliojitolea kutumika katika safu zao. Walikuja Hebroni wakiwa wameamua kikamilifu kumfanya Daudi mfalme juu ya Israeli yote. Waisraeli wengine wote walikuwa pia na nia hiyo moja ya kumfanya Daudi kuwa mfalme. 39 fWatu hawa wakakaa huko na Daudi siku tatu, wakila na kunywa, kwa sababu jamaa zao zilikuwa zimewapatia mahitaji yao. 40 gPia, majirani zao hata wale walio mbali hadi Isakari, Zabuloni na Naftali, walikuja wakiwaletea vyakula walivyovibeba kwa punda, ngamia, nyumbu na maksai. Kulikuwepo na wingi wa unga, maandazi ya tini, maandazi ya zabibu kavu, divai, mafuta, ngʼombe na kondoo, kwa maana kulikuwa na furaha katika Israeli.

Copyright information for SwhNEN